Header Ads Widget

Wahandisi Usafirishaji Wajengewa Uwezo Kusimamia Miradi kwa Ufanisi

 



Wahandisi wa sekta ya usafirishaji kutoka wizara na taasisi mbalimbali nchini wamekutana jijini Arusha kwa mafunzo maalum ya siku tano yanayolenga kuboresha usimamizi wa miradi ya miundombinu na kupunguza changamoto za gharama kubwa na ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi.


Mafunzo hayo yameandaliwa na Chama cha Barabara Tanzania (TARA) kwa kushirikiana na wataalamu wabobezi kutoka Tanzania na Zambia, ambapo mada mbalimbali za kitaalamu zinawasilishwa ili kuongeza ujuzi na ufanisi wa wahandisi hao.


Akifungua rasmi mafunzo hayo, Mhandisi Florian Kabaka, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TARURA, alisema kumekuwapo na changamoto kubwa kwenye mikataba ya miradi, ikiwemo mabadiliko ya gharama, madai yasiyokuwa kwenye makubaliano ya awali, na kasoro zinazojitokeza kutokana na ukosefu wa tathmini ya kina kabla ya utekelezaji.


> “Kumekuwa na matatizo mengi katika mikataba, mara nyingi gharama hubadilika na kuzidi bajeti, au madai mapya hujitokeza, jambo linaloigharimu serikali. Mafunzo haya yatawasaidia wahandisi wetu kusimamia mikataba kwa weledi zaidi kuanzia hatua ya ubunifu wa mradi hadi ukamilikaji wake,” alisisitiza Mhandisi Kabaka.



Aliongeza kuwa ni vyema wahandisi wasio na uzoefu wa kutosha wakasimamiwa na wataalamu wabobezi, ili kuzuia serikali kuingia hasara zisizo za lazima.


Kwa upande wake, Mhandisi Pharles Ngeleja kutoka TARURA alieleza kuwa sekta ya usafirishaji imeendelea kupanuka kwa kasi, hususan maeneo ya vijijini, ambapo miradi ya barabara na madaraja ya mawe imekuwa chachu ya maendeleo.


> “Tangu kuanzishwa kwa TARURA mwaka 2017 tumefanikisha ujenzi wa takribani madaraja 453 ya mawe, hatua ambayo imeokoa gharama kubwa kwa serikali na kufungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa wananchi wengi,” alisema Ngeleja.



Alifafanua kuwa kupitia miradi hiyo, wananchi wameweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi, kufikia huduma muhimu, na kuongeza kipato chao, hivyo kuchochea maendeleo ya maeneo ya vijijini.


Mafunzo hayo yamehusisha wahandisi kutoka OR-TAMISEMI, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Ujenzi, Mfuko wa Barabara, TARURA pamoja na TANROADS, na yanatarajiwa kuongeza mabadiliko chanya katika usimamizi wa miradi ya usafirishaji nchini.

Post a Comment

0 Comments